“
Siku moja, jambo baya litatokea. Labda babu yako au mnyama wako kipenzi atafariki au shangazi yako atagundulika na kansa. Labda utafukuzwa kazi au utaachika kwa mumeo au mkeo mliyependana sana. Labda rafiki yako kipenzi atapata ajali mbaya ya gari na utatakiwa kupeleka taarifa kwa ndugu na marafiki zake. Kutoa taarifa ya jambo baya kwa mtu ni kazi ngumu sawa na kupokea taarifa ya jambo baya kutoka kwa mtu. Kama umeteuliwa kupeleka taarifa ya kifo au ya jambo lolote baya kwa mtu fanya hivyo kwa makini. Toa taarifa ya msiba au ya jambo lolote baya kwa hekima na busara kama Ibrahimu alivyofanya kwa Sara kuhusiana na kafara ya Isaka, si kama Mbenyamini alivyofanya kwa Eli kuhusiana na kutwaliwa kwa sanduku la agano na kuuwawa kwa watoto wake wawili. Jidhibiti kwanza wewe mwenyewe kama umeteuliwa kupeleka taarifa ya kifo au ya jambo lolote baya. Angalia kama wewe ni mtu sahihi wa kupeleka taarifa hiyo. Pangilia mawazo ya kile unachotaka kwenda kukisema au unachotaka kwenda kukiandika. Mwangalie machoni, si usoni, yule unayempelekea taarifa kisha mwambie kwa sauti ya upole nini kimetokea.
”
”