β
Mbegu ni neno la Mungu. Mfano bora, msamaha, ndoto, tabasamu, uadilifu, uaminifu, uchapakazi na uvumilivu ni maneno ya Mungu. Kwa hiyo mfano bora, msamaha, ndoto, tabasamu, uadilifu, uaminifu, uchapakazi na uvumilivu ni mbegu. Watu ni ardhi. Panda mbegu ya mfano bora kwa watoto wako, msamaha kwa maadui zako, ndoto kwa malengo yako, tabasamu kwa marafiki zako, uadilifu kwa waajiri wako na kwa wafanyakazi wako pia kama unao, uaminifu kwa marafiki zako wa ukweli, uchapakazi kwa kazi zako na uvumilivu kwa wapinzani wako. Kila mbegu irutubishwe kwa imani na upendo kwa watu.
Katika mfano huu ukuaji unawakilisha utakaso, ambao ni muundo wa taswira ya Mungu ndani yetu kwa kuishi kama anavyoishi yeye kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Tunachotakiwa kufanya baada ya kupanda mbegu ni kutimiza wokovu wetu sisi wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kutimiza wokovu wetu sisi wenyewe ni sawa na mvua, jua, palizi, mbolea, ili mavuno yaweze kuwa ya uhakika.
β
β