β
Hakimu na Kuhani Mkuu wa Shilo Eli alipata matatizo makubwa wakati wa mgogoro wa Waisraeli na Wafilisti, kati ya mwaka 2871 na 2870 Kabla ya Kristo. Mara tu baada ya kupewa taarifa ya kifo cha watoto wake wawili, Hofni na Finehasi, na kutwaliwa kwa Sanduku la Agano la Bwana wa Majeshi lililohifadhi Amri Kumi za Mungu, Eli alianguka kutoka katika kiti chake na kufariki papo hapo akiwa na umri wa miaka 98. Aidha, mkwe wa Eli, mke wa Finehasi, alijifungua ghafla na kufariki alipopata taarifa ya kifo cha mkwewe na taarifa ya kuuwawa kwa mumewe na ya kutekwa nyara kwa Sanduku la Agano.
Mwanajeshi kutoka Benyamini falaula angetumia hekima na busara kutoa taarifa ya kifo na ya kutwaliwa kwa Sanduku la Agano huenda Eli asingefariki, na huenda mkwewe asingejifungua mtoto njiti na huenda asingekufa siku hiyo. Kwani Sanduku la Agano lilirejeshwa nchini Israeli, na Wafilisti wenyewe, baada ya miezi saba tangu litwaliwe, na kifo cha watoto wa Eli yalikuwa mapenzi ya Mungu. Hivyo Eli asingeweza kuzuia kifo cha watoto wake, na Wafilisti wasingeweza kukaa na Sanduku la Agano milele.
Lakini katika kafara ya Isaka ambapo Isaka aliamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake kama Yesu alivyoamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake wa mbinguni, Sara angekufa kama Ibrahimu hangetumia hekima alipomwambia anakwenda kumtolea Bwana kafara ya mwanakondoo wakati akijua anakwenda kumtoa Isaka mtoto wa pekee wa Sara. Hekima inatoka moyoni, busara inatoka mdomoni. Kwa vile suala la kutoa taarifa mbaya kwa mtu ni gumu kwa yule anayetoa na kwa yule anayepokea, hekima na busara havina budi kutumika.
β
β