“
Kesho yake Ijumaa Rais wa Meksiko alirudi kutoka Panama na aliomba kuonana na Vijana wa Tume; alitaka kuwapongeza binafsi, na kuwapa nishani za heshima kwa mchango wao mkubwa kwa Jamii ya Meksiko. Randall Ortega alilipeleka ombi hilo kwa Rais wa Tume ya Dunia; Rais wa Tume ya Dunia akakaa na Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia na kumrudishia Randall Ortega jawabu, kwamba Vijana wa Tume waliruhusiwa kuonana na Rais wa Meksiko na baadhi ya maafisa wa juu wa serikali ya shirikisho. Saa mbili usiku wa siku hiyo, Ijumaa, kulifanyika sherehe ndogo ya siri nyumbani kwao Debbie; sherehe iliyohudhuriwa na Rais wa Meksiko na mke wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Meksiko, Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Marekani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Nchini Meksiko, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maafisa wa tume na watu wengine wa muhimu katika kazi ya Vijana wa Tume.
”
”