Huzuni Quotes

We've searched our database for all the quotes and captions related to Huzuni. Here they are! All 7 of them:

Kipo kitu kinaendelea kufanyika katika siku zetu za furaha na katika siku zetu za huzuni kwa kila mmojawetu hapa duniani bila ya upendeleo wowote. Kitu hicho ni kuingia na kutoka kwa pumzi, au kupumua. Ukiithamini pumzi inayoingia na kutoka ndani ya mwili wako utapata zawadi ya amani katika maisha yako. Utapata pia zawadi ya furaha, uelewa na ufasaha! Ijapokuwa una matatizo mengi katika maisha, kitu bora cha kufanya ni kushukuru Mungu kwa maana wewe ni mzima.
Enock Maregesi
Marafiki zako wa mwanzo ambao bado ni marafiki zako mpaka sasa ni wazuri kuliko wote kutokana na sababu mbalimbali: Wamekuwepo pamoja nawe katika shida na raha; wanakujua vizuri unapokuwa na furaha, na wanakujua vizuri unapokuwa na huzuni; mmezoeana kwa miaka mingi na wanaujua hata utani wako wa ndani; wanajua nini unapendelea zaidi na nini hupendelei zaidi, na wanazijua sifa zako za ushupavu na sifa zako za udhaifu. Hata hivyo, katika maisha yetu, tunahitaji marafiki wa aina zote mbili kurahisisha maisha. Marafiki wapya hutuongezea viungo muhimu katika maisha yetu wakati marafiki wa mwanzo ni nguzo au miamba imara ya maisha yetu, na ndiyo watu hasa watakaotusaidia katika shida na raha! Usiwapoteze au usiwaache marafiki zako wa mwanzo lakini jenga mahusiano mapya. Marafiki zako wa mwanzo ni dhahabu, wa sasa ni fedha.
Enock Maregesi
Ningependa kujitokeza leo kutoa salamu zangu za rambirambi kwa Watu wa Musoma; kutokana na ajali mbaya ya mabasi ya J4 Express, Mwanza Coach, na gari ndogo aina Nissan Terrano, iliyotokea Ijumaa tarehe 5/9/2014 katika eneo la Sabasaba mjini Musoma. Kulingana na vyombo vya habari, watu 39 wamefariki dunia. Wengine wengi wamejeruhiwa vibaya. Mali za mamilioni ya fedha zimeteketea kabisa. Hii ni ajali mbaya na ya kusikitisha mno kwa maana halisi ya maneno mabaya na ya kusikitisha. Maneno hayataweza kuelezea kikamilifu huzuni niliyonayo juu ya ajali hii ya kutisha, lakini Mungu awasaidie wale wote waliofiwa au walioguswa na ajali hiyo kwa namna yoyote ile, na awasamehe marehemu wote dhambi zao na awapumzishe mahali pema peponi. Wale wote waliofariki hawataweza kurudi huku, lakini sisi tutakwenda huko.
Enock Maregesi
Kuna ndoto za mchana na kuna ndoto za usiku. Ndoto za mchana ni maono ya kile ambacho roho inatamani kuwa. Ndoto za usiku ni maono yanayotokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira; ukiota kuhusu maji, hiyo ni ishara ya siri; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni; ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio. Kitu cha kwanza kufanya unapoota ndoto za kishetani, utakapoamka, mwombe Mungu akunusuru kutoka katika matatizo yoyote yanayokunyemelea; au yanayomnyemelea mtu mwingine yoyote yule, hata usiyemjua. Ubongo ni kitu cha ajabu kuliko vyote ulimwenguni na umetengenezwa na Mungu. Ndoto zinapatikana ndani ya ubongo. Ubongo unapatikana ndani ya ufahamu. Ufahamu mtawala wake ni malaika mwema. Malaika mwema anajua siri ya ndoto. Kila mtu anaota na kila ndoto ina maana yake. Rekodi ndoto zako kila siku kwa angalau mwezi mzima kupata maana halisi ya ndoto hizo, na kujua kwa nini ulizaliwa.
Enock Maregesi
Taabini hii ni ngumu sana kwangu kuandika pamoja na kwamba ni miaka mitatu kamili toka giza liingie. Mwaka 2014, Novemba 4, nilimpoteza bibi yangu mpendwa, Martha Maregesi, aliyefariki dunia kutokana na ukongo wa kiharusi, na tutamkumbuka daima. Alikuwa na roho ya kipekee; na kifo chake kiliwagusa wengi, pamoja na kwamba aliishi maisha kamili, zaidi ya siku 25550, siku 5110 zaidi, ambazo ndizo tulizopangiwa na Mungu. Mapenzi ya mtu kwa bibi yake ni mapenzi ya kipekee. Nadhani Mungu aliwapa mabibi wote uwezo maalumu wa kuwapenda wajukuu zao, na kufanya maisha yao yatimie, kuwafanya wawe binadamu wazuri na wenye maadili mema. Alichangia pakubwa katika malezi yangu ya utotoni; na aghalabu naweza kukumbuka nikiwa naye jikoni akipika, huku mimi nikifanya kazi nyingine, lakini wakati huohuo akinifundisha mambo kadha wa kadha ya kunikomaza kimaisha. Bibi hakuwa tu bibi. Alikuwa mlezi, rafiki na mtu aliyenihamasisha sana katika maisha. Kifo kinaleta huzuni lakini kinaleta tumaini. Naamini bibi yangu atakwenda mbinguni, kwa sababu naamini alitubu dhambi zake akisaidiwa na wachungaji. Wachungaji hao walimtembelea kila siku, nyumbani au hospitalini, akiwa kitandani kwake akiugua. Bibi yangu alitimiza wajibu wake. Alizaliwa, aliishi, na alikufa katika toba. Siku nitakapokufa ningependa kuzikwa jirani na alipozikwa bibi yangu, ili Yesu atakaporudi tufufuke pamoja.
Enock Maregesi
Marafiki wanaweza kukupotosha bila wao wenyewe kujua na bila kuwa na nia mbaya ya aina yoyote ile; na wanaweza kuwa washauri wazuri kwa sababu wanakujua vizuri unapokuwa na huzuni, na wanakujua vizuri unapokuwa na furaha pia. Kwa mfano; rafiki yako anaweza kukushauri kusomea uhasibu wakati Mungu amekupangia utawala, au anaweza kujua aongee na wewe wakati gani kulingana na tabia yako ya kubadilikabadilika. Maadui wanasaidia kujua kipaji ulichopewa na Mungu – ukifanya kitu ambacho si cha kawaida katika maisha yako halafu ukawa na maadui ujue hicho ndicho Mungu alichokupangia kufanya, hivyo usikate tamaa – na mashabiki wanasaidia kufanya kipaji chako kiwe na uhai.
Enock Maregesi
Aidha, tunaweza kupata inkishafi kutokana na asili ya miili yetu, matukio fulani ya wakati ujao yana asili yake katika ndoto za binadamu. Ndoto hizo au maono hayo ni ishara ya kile kinachokuja mbele katika maisha ya mtu; kama vile afya, ugonjwa au hatari. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira – unatakiwa kuwa na hekima; ukiota kuhusu mimba na unajifungua, hiyo ni ishara ya kuwa katika mchakato wa kutengeneza wazo jipya – unatakiwa kushukuru; ukiota unaruka angani, hiyo ni ishara ya tumaini – unatakiwa kushukuru; ukiota kuhusu maji au kiowevu kingine chochote kile, hiyo ni ishara ya siri na wakati mwingine ni ishara ya kuwa na matatizo ya kiafya kama utaota kuhusu maji machafu – unatakiwa kuwa msiri na msafi; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni – unatakiwa kuomba; na ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio – unatakiwa kushukuru.
Enock Maregesi